MAMIA YA WANANCHI WAMEJITOKEZA KATIKA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA KUTOKA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO INAYOFANYIKA MKOANI GEITA.
Posted on: November 4th, 20237 Novemba,2023.
Zaidi ya wananchi 250 wamejitokeza kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya watoto, magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya mifupa na viungo, magonjwa ya upasuaji katika kambi maalumu ya matibabu inayofanywa na Madaktari bingwa na Wataalamu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya Mkoa wa Geita.
Katika kutekeleza agizo la Wizara ya Afya chini ya Mhe.Ummy Mwalimu, serikali imeagiza hospitali za kanda kuhakikisha zinawafikia wananchi kwa kusogeza huduma za kibingwa na bingwa bobezi karibu yao na hadi sasa Hospitali za Rufaa ya Kanda Chato imetekeleza agizo hili na imefanikiwa kuzifikia hospitali 3 ndani ya Tanzania na kufanikiwa kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 2000.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH), Dkt. Oswald Lyapa, Mratibu wa huduma tiba na Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake amesema; "Kambi hii ya uchunguzi na matibabu ya kibingwa ni muendelezo wa huduma mkoba yenye lengo la kuwafikia maelfu ya wananchi ambao muda mwingine kupata huduma hizi za kibingwa na bingwa bobezi ni ngumu kutokana na sababu mbalimbali, hivyo kwa hospitali yetu ya CZRH tunaendelea kuwafikia ili wanufaike na matibabu ya kibingwa kama sehemu ya lengo la Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Na katika kulitimiza hili tumeendelea kuwabaini mapema hasa wale wanaosumbuliwa na magonjwa sugu hivyo kuwaanzishia matibabu na ufuatiliaji wa karibu kwa nia ya kuokoa maisha yao."
Zaidi ya wananchi 1000 wanategemewa kufanyiwa uchunguzi na matibabu katika kambi hii ya siku tano itakayo hitimishwa Novemba 10 katika Hospitali ya Mkoa wa Geita. Hadi kufikia sasa changamoto za afya ambazo zimebainika ni pamoja na; changamoto ya uzazi hasa kwa wanawake, na kwa upande wa watoto wengi wamegundulika kuwa na changamoto ya lishe pamoja na matatizo ya akili kwa kitaalamu ( cerebral palsy) na Wataalamu wanatumia nafasi hii ya huduma mkoba kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya mitindo bora ya maisha kuepukana na magonjwa haya.