MSD, JKCI KUANZA UJENZI WA VITUO VYA UTOAJI HUDUMA NDANI YA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO(CZRH) MAPEMA MWAKA HUU

Posted on: September 11th, 2024

Timu ya Viongozi na wawakilishi kutoka Bohari ya Dawa (MSD) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) leo Septemba 11,2024 wamefika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kwa ajili ya kukagua maeneo yaliyoandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa ghala la utunzaji dawa, kiwanda cha uzalishaji vifaa tiba pamoja na jengo la upasuaji wa moyo vitakavyoendeshwa chini ya taasisi hizi mbili.


Akizungumza mara baada ya kutembelea maeneo hayo, Meneja wa MSD Kanda ya Kagera, Bw.Kalendero Masatu amesema, “Bohari ya dawa inatambua umuhimu wa uwahishwaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya hivyo tumeridhia mpango wa kuanza ujenzi wa ghala la utunzaji dawa na vifaa tiba pamoja na kiwanda cha uzalishaji dawa na vifaa hapahapa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.Hii ni kwaajili kurahisisha usambaji wa bidhaa hizi katika maeneo ya kanda ya ziwa.Kukamilika kwa ujenzi huu unaenda kuleta maboresho ya huduma kwa wateja, upatikanaji wa bidhaa ghalani, usambazaji wa bidhaa kwa wakati ili kuendelea kuimarisha afya za wananchi.


Aidha, Eng. Baltazal Swai kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ameishukuru Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kwa kuendelea kuwa wajumbe wazuri katika kuhamasisha na kuibua wagonjwa wapya wenye matatizo ya moyo kanda ya ziwa na sasa hospitali inashirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kuendesha kliniki ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.Eng.Swai ameongeza na kusema “Kwa kulitambua hili, Serikali imeamua kutekeleza azimio hili la ujenzi wa jengo la utoaji huduma za uchunguzi, upasuaji na matibabu ya magonjwa ya moyo ndani ya hospitali hii na ujenzi huu utaanza mapema kufikia mwaka 2025 na huduma zote zinazopatikana katika Taasisi yetu ya JKCI zitapatikana hapa.


Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Dkt. Brian C. Mawalla, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuazimia na kutenda vile hospitali hii ilipangwa kujengwa.


“Ujenzi wa Jengo la Upasuaji moyo (Cathlab) chini ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, unaenda kutusaidia sisi wananchi wa kanda ya ziwa ambao tulilazimika kuzifuata huduma hizi Dar es Salaam na sasa kliniki ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo na upasuaji wa mishipa ya damu tumeishaanza ambapo kila wiki ya tatu ya mwezi tunafanya kliniki hii tukishirikiana na Madaktari bingwa na bobezi kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kwa Mwezi huu wa Septemba, kliniki ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambayo itafanyika na Madaktari bingwa na bobezi kutoka JKCI watashirikiana na wenzao wa hapa Hospitali ya Kanda ya Chato. Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la upasuaji unaenda kufanya huduma zote ambazo wananchi husafiri kwenda mbali sasa watazipata hapa Chato”

Sambamba na hilo Dkt.Mawalla amesema, kituo cha MSD cha utunzaji na uzalishaji dawa na vifaa ndani ya hospitali hii itatufanya kuendelea kuimarisha huduma kama ambavyo hospitali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha dawa zote muhimu zinapatikana muda wote.

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.