MWENYEKITI WA TUGHE TAIFA ATEMBELEA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO.
Posted on: May 6th, 2024Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) CDE. Joel G. Kaminyonge, leo Mei 6, 2024 ameitembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) na kufanya mazungumzo na Watumishi kutoka katika kada mbalimbali.
Mwenyekiti Kaminyonge ametembelea hospitali kwa lengo la kuzungumza na wanachama, kupokea na kuratibu changamoto wanazokutana nazo katika utendaji kazi na maslahi ili kuwasaidia wanachama hawa kufanya kazi katika mazingira yanayowapa unafuu wa kuweza kutoa huduma za afya kwa weledi ili kutimiza ahadi ya viapo vya taaluma zao.
Ameipongeza Menejimenti na Watumishi chini ya Mkurugenzi Dkt. Brian C. Mawalla kwa kuhakikisha taasisi inakuwa moja ya kituo cha utoaji huduma za afya hasa katika upimaji na uibuaji wa wagonjwa wapya wanaogundulika kuwa na magonjwa ya moyo katika Kanda ya Ziwa na hivyo kuwasaidia Wananchi kutambua hali zao mapema ili kuanza matibabu mapema.
CDE. Kaminyonge amesema “Mwanzo sikuwa nafahamu kama Hospitali ya Kanda Chato inatoa huduma za magonjwa ya moyo, nimefuatilia hili na kuambiwa hospitali hii ni ya kanda na tegemeo la wananchi wa kanda ya ziwa, na si kanda ya ziwa tu hadi kanda ya magharibi na nje ya nchi kama Burundi ambapo mmekuwa mkipokea wageni na wananchi wanaokuja kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo na tuna imani mtaweza kufikia lengo la uanzishwaji na kuendelezwa kwa hospitali hii”
Mwisho, CDE. Kaminyonge ameshukuru uongozi wa hospitali kwa kufanya kazi bega kwa bega na chama ikiwa ni pamoja na motisha kwa tawi la chama cha TUGHE ambayo imechangia kuimarika kwa huduma pamoja na utendaji kazi katika uokoaji wa maisha ya wananchi, hivyo kwa kutambua mchango huu chama kimetoa hati ya pongezi kwa hospitali kutambua mchango wake pamoja na ushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani 2024.